AFYA Mkoa hivi sasa una Hospitali tisa (9), Zahanati 199 na vituo vya Afya 22. Huduma ya Afya mkoani hutolewa kwa ushirikiano mkubwa baina ya Serikali na Sekta binafsi. Mashirika ya dini yanamiliki hospitali sita (6), Vituo vya Afya sita (6) na Zahanati 30. Aidha watu binafsi wanamiliki zahanati nane (8) na Taasisi za Serikali zinamiliki zahanati mbili (2).
Kulingana na huduma zilizopo, Mkoa unakabiliwa na uhaba mkubwa wa madaktari bingwa na wa kawaida hasa katika Hospitali zote za Serikali. Uwiano uliopo kati ya Daktari na mgonjwa ni 1:36,624 wakati uwiano wa kitaifa ni 1:25,000.
Pamoja na kuwa na upungufu wa madaktari, tunashukuru kwa uamuzi wa Serikali wa kuongeza maslahi kwa Watumishi wa sekta ya afya kwani hivi sasa wataalam wengi wanapenda kuajiliwa Serikalini. Hivyo tunaamini pamoja na utaratibu wa kuajiri wataalam wa Afya moja kwa moja toka vyuoni utasaidia katika kupunguza tatizo hili.
Huduma za afya zinazidi kuboreshwa kupitia mfuko wa pamoja wa afya ambao umewezesha kukarabati Hospitali, zahanati na vituo vya afya katika Halmashauri. Vile vile katika mwaka wa Fedha 2007/2008 mkoa umepata shs. 600,000,000/= kwa ajili ya kuifanyia ukarabati mkubwa hospitali ya Mkoa.
Ugonjwa wa UKIMWI:
Hali ya ugonjwa wa UKIMWI Mkoani bado ni tatizo. Kutokana na utafiti ulifanywa na idara kuu ya Takwimu ikisaidiana na TACAIDS mwaka 2003/2004, ulibaini kuwa maambukizo ya UKIMWI Mkoani Ruvuma ni 6.8% KE 6.4% na ME 7.4%. Taarifa kutoka vituo mbalimbali vya afya, Zahanati na Hospitali kupitia taarifa za Wilaya; Januari hadi Desemba 2006 zinaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi Mkoani Ruvuma kwa waliojitokeza kuchangia damu ni 12.2%.
Kwa mwaka wa fedha wa 2007/2008 Mkoa pamoja na Halmashauri zake zimetenga fedha kiasi cha shilingi 533,527,000 kwa ajili ya kukabiliana na janga la UKIMWI kwa kufanya shughuli mbalimbali hususan kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu hasa yatima ambao wazazi wao wamefariki kutokana na janga la UKIMWI kwa kuwasaidia kulipa ada za shule pamoja na kuwanunulia vifaa muhimu kwa ajili ya masomo, kuzisaidia kaya zinazoongozwa na wazee wasiojiweza ambao wanalea yatima waliotokana na wazazi waliofariki kutokana na UKIMWI; Kuendelea Kutoa mafunzo kwa kamati za UKIMWI za kata na vijiji; kuendelea kutoa elimu ya kuhamasisha jamii kupima na kujua hali ya afya zao. Pia ushirikishaji jamii katika kubuni mbinu shirikishi za kupambana na janga hili.
|