Kama sote tunavyofahamu malengo yaliyomo katika MKUKUTA ni yale yale ambayo yamo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005. Lengo kuu ni kuboresha maisha ya kila Mtanzania. Sisi Wana-Ruvuma tulijiuliza swali hili; Je! Tutaboreshaje hali ya maisha ya kila Mwana-Ruvuma? Je Mkoa utashiriki vipi katika kuchangia ukuaji wa uchumi (GDP) kufikia asilimia 8 hadi 10 kwa mwaka 2010? Je kuongeza ushiriki wa Sekta Binafsi unakuaje?
Moja ya malengo ya MKUKUTA ni kukuza uchumi na kuongeza kipato cha kila mwananchi. Ili tuweze kuboresha maisha ya Watanzania wote MKUKUTA unaelekeza kuwa ni lazima tuhakikishe kuwa uchumi wetu unakua kwa viwango vikubwa. Kwa mfano kuongeza ukuaji wa viwandani kutoka asilimia 8 hadi 15 kufikia mwaka 2010, kilimo kutoka asilimia 8.6 hadi 15 mwaka 2010.
Ili uchumi uweze kukua kwa viwango vikubwa ni lazima kuongeza uzalishaji. Uzalishaji katika Taifa lolote lile unaweza kuongezeka endapo watu wake wana elimu nzuri, afya nzuri, chakula cha kutosha, makazi bora na mavazi bora. Hilo ni lengo la pili la MKUKUTA wa kuwa na Ustawi wa Jamii yote.
Lengo la tatu la MKUKUTA ni Utawala Bora. Utawala wa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi, Utawala unaozingatia Uwazi na Ukweli.
Viongozi wa Mkoa wa Ruvuma tunao uwezo wa haya mawili ya kuona kuwa hali bora ya maisha ya jamii na utawala bora vinakuzwa na kuendelezwa. Lakini katika eneo la kuongeza kasi ya kukua uchumi, hili ni suala la Sekta Binafsi. Kwa hiyo Mkutano huo ulikuwa na lengo la kufunua macho ya Sekta Binafsi ili kuona wapi katika Mkoa huu wanaweza kuwekeza iwe katika miradi ya ukubwa wa aina zote (chini, kati au juu). Mchanganyiko wa Miradi ya namna hii itaongeza kwa kiasi kikubwa kiwango cha ukuaji wa uchumi hapa Mkoani Ruvuma. Kwa hiyo Mkutano huo ulisaidia kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika Mkoa huu katika nyanja za kilimo, madini, utalii, uvuvi, ufugaji na huduma na hivyo kuvutia uwekezaji.
Tunaamini kuwa tukiweza kuwavutia wawekezaji wengi zaidi tutaweza kuongeza siyo tu pato la kila mwananchi aishiye Mkoani Ruvuma, bali pia pato la Taifa zima.
Tunategemea kuwa uwekezaji katika Mkoa wa Ruvuma utatuwezesha kuongeza uzalishaji wa bidhaa za viwanda na kilimo kwa ajili ya kuuza ndani ya nchi na nchi za SADC, Afrika Mashariki na soko la AGOA
Katika mkutano huo shughuli za Madini, Uvuvi, Utalii na Ufugaji wa kisasa ziliweza kuibuliwa na hivyo kuwafanya wawekezaji wengi waone umuhimu wa kuwekeza katika Mkoa huu.
Back Next |