Rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania Mh. Benjamin William Mkapa amefaidhaishwa na kitendo cha baadhi ya viongozi wanaopenda kusema kuwa watawaletea wananchi Maendeleo kwani dhana hii ni potofu na inayofifisha jitihada za wananchi kujiletea Maendeleo. Rais mstaafu Mh. William Mkapa ameyasema hayo jana tarehe 9/06/2011 wakati akitoa salamu zake katika ibada ya jubilee ya kutimiza miaka ishirini na tano ya Askofu mkuu wa Kanisa la Katoliki jimbo kuu la Songea mkoani Ruvuma.
Rais mstaafu ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi amesema viongozi wa ngazi zote hawapaswi kusema ya kuwa watawaletea wananchi Maendeleo badala yake washirikiane kuwaongoza watu katika kujieletea Maendeleo yao.
Amesema ni budi sote tukafahamu kuwa wananchi wanajua namna ya kujiongezea kipato chao na kinachokwamisha ni michango kutoka kwa watu wengine au viongozi kwani maendeleo ni budi yakaletwa na wananchi wenyewe.
Alimnukuu Baba wa Taifa hayati mwalimu Julius Nyerere kwa kusema “Maendeleo ni jukumu letu wenyewe na yatatokana tuu na jitihada zetu pasipo kutegemea wafadhili” alisema rais mstaafu Mkapa
Amewasihi wote wanaopenda kuona Maendeleo kutembelea Jimbo Katoliki la Songea na Mbinga kuona namna watu waliosaidiwa kujiendeleza walivyoweza kujiendeleza.
Alitumia nafasi hiyo kusisitiza suala la Amani hapa nchini hususan kipindi hiki nchi inaposherehekea miaka hamsini ya Uhuru.
Aidha Rais mstaafu huyo amewaomba viongozi wa dini nchini kuiombea nchi ya Sudan ambayo imepata kukubali kugawanyika na upande wa Sudan Kusini kuanzisha Taifa kuiombea ili Amani ipatikane.
Ameongeza kusema aliteuliwa na Umoja wa Mataifa kusimamia mchakato wa kura ya maoni nchini Sudan na anategemea sana kuona nchi hiyo inasitisha mauaji ya raia wasiokuwa na kosa na kuondoa uhasama wa kikabila .
Amesema inasikitisha kuona kwa kipindi kifupi kati ya Januari mwaka huu hadi sasa zaidi ya watu elfu moja wamepoteza maisha kusini mwa Sudan.
“Nawaombeni sana mjumuike nami katika sala ili hawa ndugu wa Sudan kusini wapate Amani ya kudumu” alisema Rais mstaafu na kuongeza kuwa nuru hii iliyotuangazia sisi watanzania iwaangazie viongozi wa Sudan ili watekeleze kwa msingi uamuzi wao wa kuleta Amani.
Wakati huo huo Rais mstaafu Mkapa amempongeza Askofu mkuu Norbert Mtega wa jimbo la Songea kwa kuwa mwanaharakati mahili wa kupigania elimu nchini ambapo katika kipindi cha miaka hii ishirini na tano amefanikisha kuanzishwa kwa vyuo vikuu vya Ruaha na chuo kikuu cha kilimo cha Songea.
Amemsifu Askofu mkuu Norbert Mtega kwa kumweleza kuwa ni “ mwalimu,kuhani na mchungaji mwema” hivyo asichoke kuhubili injili na kuwasaidia wote wanaohitaji Huduma na maelekezo yake.
Askofu Mkuu Norbet Mtega ni askofu wa pili wa jimbo kuu la Songea baada ya hayati askofu mkuu Yakobo Komba alizaliwa tarehe 17 Agosti 1945 katika parokia ya Lupanga jimbo la Njombe.
Alisoma falsafa na Tauhidi katika seminari kuu ya Peramiho kuanzia mwaka 1968 mpaka 1973.Alipatiwa sakramenti ya daraja la takatifu la Upadre mwaka 1973 na aliwekwa wakfu na kusimikwa kuwa askofu wa wa Jimbo la Iringa huko Roma tarehe 06 Januari 1986 na mwenye heri Papa Yohane Paulo II .
Na ilipofika tarehe 06 Julai 1992 aliinuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Songea hadi hii leo anapotimiza jubilee ya miaka ishirini na tano ya Uaskofu.
Misa hii imehudhuriwa na maaskofu wote wa Kanisa Katoliki nchini pamoja na wageni mbalimbali wakiongozwa na Rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Benjamini William Mkapa,Mama Anna Mkapa na mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Christine Gabriel Ishengoma.
Picha ya kushoto Rais mstaafu Benjamin Mkapa akiwa na Mama Anna Mkapa wakati wa ibada ya misa ya jubilei ya miaka ishirini na tano ya Askofu mkuu Norbet Mtega wa Jimbo kuu katoliki la Songea. Picha ya Kushoto Askofu mkuu Norbert Mtega akizungumza na waumini waliohudhuria jubilei yake ya kufikisha miaka ishirini na tano ya uaskofu.Chini Rais mstaafu Mh. Mkapa akiwa katika picha ya pamoja na Askofu mkuu Norbert Mtega (kushoto) na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo (kulia) na wakwanz kulia ni mkuu wa Mkoa wa Ruvuma dkt.Christina Ishengoma na Mama Anna Mkapa na maaskofu wamesimama kwa nyuma.

|