HIFADHI YA MAZINGIRA, MALIASILI NA MISITU
Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa Mikoa michache ambayo uoto wake wa asili haujaharibiwa. Jitihada zinaendelea kufanyika kulinda uoto huu usiweze kuharibiwa kutokana na shughuli za wanadamu.
Eneo la misitu iliyohifadhiwa ni kilometa za mraba 7,128. kati ya eneo hilo kilometa za mraba 6,958 ni hifadhi za Taifa na 170 ni hifadhi za Halmashauri. Eneo lililohifadhiwa ni asilimia 11 ya eneo la Mkoa. Maeneo mengine yapo katika mchakato wa kutengwa kama hifadhi za vijiji na Halmashauri chini ya Mradi Maalum wa Misitu Shirikishi Jamii (Participatory Forest Management) ulioanza katika mwaka wa fedha 2005/2006. Maeneo hayo pia yanahusisha vyanzo vya maji.
Katika kuyarudishia hali yake ya asili maeneo yaliyoachwa wazi baada ya kukatwa miti, katika mwaka 2006/2007 imepandwa miti 6,000 katika eneo la hekta 3,824. Miti iliyopandwa ni Migwina, Minyenda na miti ya matunda.
Nyuki na Samaki :
Kuwepo kwa misitu mingi ya asili kunatoa fursa nzuri kwa ajili ya ufugaji wa nyuki. Idadi ya mizinga iliyopo ni 49,618 ambayo katika mwaka 2006 ilitoa asali ya uzito wa kilo 15,345 yenye thamani ya Shs.25,779,600/= na nta kilo 7,160 yenye thamani ya Shs.4,296,000/=. Mikakati ya Mkoa katika kuendeleza sekta hii ni pamoja na kuimarisha mizinga ya kisasa pamoja na kutoa elimu kwa warina asali.
Kwa upande wa samaki, Mkoa unategemea Ziwa Nyasa, mito na mabwawa. Hata hivyo tija kutokana na vyanzo hivyo vya samaki havitoshelezi mahitaji ya Mkoa. Kutokana na hali hiyo Mkoa unapata pia samaki kutoka nje ya Mkoa. Katika mwaka 2006 kilo 628,585 zenye thamani ya shs.628,585,000/= ziliuzwa Mkoani Ruvuma.
Wanyamapori:
Wanyamapori ni raslimali muhimu inayotegemewa Mkoani Ruvuma. Hii kwa sababu ya kuwepo kwa idadi kubwa ya wanyamapori. Hivyo kutoa fursa nzuri kwa uwindaji wa kitalii ambao hufanyika katika vitalu 13 ambavyo kwa mwaka 2006 viliingizia Taifa dola za Kimarekani 231,410 sawa na Shs.293,890,700/=.
|