SHERIA
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Jamhuri ya umoja ambayo iko chini ya demokrasia ya Bunge la vyama vingi vya siasa. Mamlaka yote katika Jamhuri ya Muungano yanaendeshwa na kudhibitiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar . Kila Serikali ina nguzo tatu za utawala ambazo ni: Serikali, Mahakama na Bunge. Vyombo hivi vitatu vya utawala vina uwezo na madaraka ya kusimamia shughuli zote za umma. Aidha Mamlaka za Serikali za Mitaa huwa zinazisaidia Serikali hizi kuu mbili katika shughuli zake za kutawala nchi. Serikali ya Jamhuri ya Muungano ndiyo yenye mamlaka yote yanayohusu shughuli za Muungnao pamoja na zile za Tanzania Bara wakati ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina mamlaka tu kuhusu mambo ya Tanzania Visiwani ambayo hayako chini ya makubaliano ya Muungano. Serikali
Rais wa Jamhuri ya Muungano ndiye mkuu wa Nchi, Mkuu wa Serikali na kamanda Mkuu a Majeshi. Viongozi ambao wako katika Mamlaka kuu ya Nchi ni Rais wa Jamhuri, Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu na Baraza la Mawaziri wa Jamhuri ya Muungno wa Tanzania.
Rais ndiye kiongozi Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Makamu wa Rais ndiye msaidizi mkuu wa Rais kuhusu masuala yote ya Jamhuri ya Muungano. Hususan anamsaidia Rais katika kusimamia utekelezaji wa shughuli za kila siku za Muungano, kutekeleza kazi zozote atakazoagizwa na rais pamoja na kuchukua madaraka ya Urais wakati Rais mhusika hayupo madarakani au akiwa amesafiri kwenda nje ya nchi. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya muungno ndiye Kiongozi mkuu wa shughuli za Serikali Bungeni, na amepewa mamlaka ya kudhibiti na kusimamia utekelezaji wa shughuli za kila siku za Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Aidha anatekeleza maagizo yoyote atakayopewa na Rais. Rais wa Zanzibar ndiye kiongozi mkuu wa Serikali ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano, akiwemo Waziri Mkuu, linateuliwa na Rais kutokana na Wabunge wa Bunge la Muungano. Serikali inatekeleza majukumu yake ya kila siku kupistia Wizara ambazo zinaongozwa na Mawaziri. Kila Wizara imepewa majukumu yake katika sekta mbalimbali.
Mahakama
Shughuli za Mahakama Tanzania zinahusisha vyombo vitatu, ambavyo ni: Mahakama ya Rufaa ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Mahakama Kuu za Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, Tume ya Huduma za Sheria Tanzania pamoja na mahakama za chini Tume ya Huduma za Sheria Tanzania Bara in wajumbe watano, ambao ni: Jaji Mkuu wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania (Mwenyekiti), Jaji mmoja wa Mahakama Kuu ya Rufaa ya Tanzania, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu na wajumbe wengine wawili wanaochaguliwa na Rais.
Mfumo wa Sheria
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) katika utangulizi wake inaeleza wazi kuwa wananchi wa Tanzania wameamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yao jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani. Misingi hiyo yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye demokrasia ambayo Serikali yake husimamiwa na Bunge lenye wajumbe waliochaguliwa na linalowakilisha wananchi, na pia yenye mahakama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga wala upendeleo wowote, na hivyo kuhakikisha kwamba haki zote za binadamu zinadumishwa na kulindwa, na wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu.
Kwa madhumuni haya basi, Katiba ya Jamhauri ya Muungano wa Tanzania , 1977, katika kifungu chake cha 4, inaeleza kwamba shughuli zote za mamlaka ya Nchi katika Jamhuri ya Muungano zitatekelezwa na kudhibitiwa na vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki, na pia vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma. Vyombo vyenye mamlaka ya utendaji vitakuwa ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; vyombo vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki vitakuwa ni Idara ya Mahakama ya Serikali ya Jamhuri ya Muungnao na Idara ya Mahakama ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na vyombo vyenye mamlaka ya kutunga Sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma vitakuwa ni Bunge na Baraza la Wawakilishi. Source: http://www.tanzania.go.tz/utawalaF.html |