Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe.Agnes Richard Kayola amefanya ziara rasmi ya Kikazi Wilayani Nyasa kwa lengo la kuona fursa za uwekezaji,raslimali zilizopo na kukiri kuwa iwapo zitatumiwa vyema zinaweza kuchechemua uchumi kuanzia ngazi ya Kaya.
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mhe.Peres Boniphace Magiri akiwasilisha taarifa kwa Mhe.Balozi Kayola amesema uchumi wa Nyasa kwa 75% unatokana na Kilimo cha mazao ya chakula kama Mahindi,maharage,Karanga na Mazao ya biashara ikiwemo Kahawa na Korosho kwa uchache
Mhe.Magiri ameongeza kuwa sehemu ya uchumi inatokana na Uvuvi kutokana na uwepo wa Ziwa Nyasa,uchimbaji wa madini,Utalii wa kisiwa cha Lundo huku akibainisha fursa mpya za uchumi kama usafiri na usafirishaji,usindikaji wa Mazao ya ziwani, uwekezaji wa hoteli kutokana na uwepo wa fukwe kando ya ziwa Nyasa,usambazaji na uuzaji wa bidhaa za viwandani,usindikaji wa Matunda na usindikaji wa Mazao ya Kilimo.
Akiongea na wafanyabiashara Mhe.Balozi Kayola amewataka kuwa wazalendo kwa kuzitangaza na kutumia fursa zilizopo nchini, kuangalia hali ya ulinzi na Usalama ili kufanyabiashara zao bila Vikwazo na kulinda mitaji yao,kuzitumia fursa za Mazao kwa kufuata Sheria na taratibu zilizopo na fursa za usafiri na usafirishaji
Aidha,Mhe.Balozi Kayola ametoa rai kwa Watanzania kuendelea kuchapa kazi kuiunga mkono Serikali iliyopo Madarakani kwa vitendo kwa uthubutu wa Kujenga Bandari kubwa inayogharimu kiasi cha fedha zaidi ya Shilingi bilioni 80 kwani inakwenda kuchagiza Sekta ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kwa mataifa ya Malawi, Msumbiji, Zambia na Tanzania na kuimarisha zaidi maeneo ya Kimkakati ikiwemo Viwanda, Bandari,bidhaa za Mazao na bidhaa za usindikaji.
Wakiongea kwa niaba ya wafanyabiashara Vincent Muli na Gabliel Mathius wamemwomba Mhe.Balozi kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Malawi kuboresha Mazingira ya Kibiashara ili kuwarahisishia wafanyabiashara ikiwemo Kujenga Soko la Kimataifa Wilayani Nyasa ili nchi jirani za Msumbiji,Malawi na Zambia kuja kuchukua na kuleta bidhaa.
Afisa Uhamiaji Wilaya ya Nyasa Albert Masao ametoa wito kwa wafanyabiashara kufanyabiashara halali ikiwemo kuingia kwenye mipaka ya mataifa mengine kisheria wakiwa na hati za Kimataifa za Kusafiria badala ya kutumia hati za dharula.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Nyasa Khalid A.Khalif amewataka wafanyabiashara kushirikiana na mamlaka zinazowahudumia ikiwemo Ofisi za biashara za Wilaya na Mamlaka ya Mapato ili kupata Suluhu ya Mambo yao.
Mhe.Balozi Kayola akiwa Wilayani Nyasa ametembelea fukwe zilizopo kandakando ya ziwa Nyasa,Kisiwa cha Lundo,eneo la uwekezaji la Bio Camp,Ujenzi wa Bandari kubwa inayogharimu fedha za kitanzania zaidi ya Bilioni 80,Ofisi za Uhamiaji pamoja na kuongea na wafanyabiashara.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.