Katika historia ndefu ya mapambano dhidi ya ukoloni barani Afrika, majina ya viongozi mashuhuri kama Mkwawa wa Wahehe Kinjeketile Ngwale wa Vita ya Maji Maji, na Samory Touré wa Afrika Magharibi yameandikwa kwa wino usiofutika.
Hata hivyo, kusini mwa Tanzania kuna jina moja lililosahaulika kwa muda mrefu lakini lenye uzito wa kipekee: Chifu Nduna Baina Mkomanile.
Huyu alikuwa mwanamke shujaa, mtabibu na mtawala pekee mwanamke aliyeinua sauti ya kupinga dhuluma za Wajerumani,makazi yake yalikuwa katika bwawa hili katika kijiji cha Kitanda Tarafa ya Undendeule, wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma mwishoni mwa karne ya 19.
Ni simulizi ya mwanamke jasiri aliyethubutu kusimama kidete katika enzi ambazo wanawake walionekana wanyonge, akawa nembo ya ujasiri, hekima na mapambano ya ukombozi.
Maisha Yake Kabla ya Uongozi
Kabla ya kupewa jina la utawala, aliitwa Baina. Alijulikana zaidi kama mganga wa tiba asili na mtaalamu wa unajimu. Umaarufu wake ulivuka mipaka ya Undendeule na kumfanya awe maarufu kati ya makabila jirani ya Wangoni, Wayao, Wamatengo, Wabena na Wangindo.
Urembo wake ulivutia wengi, lakini hatimaye aliolewa na Chifu Pambuka, mtawala wa ukoo wa Fussi wa Kitanda (Kutisa). Kupitia ndoa hii, Baina alipewa jina jipya: Mkomanile – jina lililoashiria heshima na mamlaka.
Pambuka alikuwa na wake wawili na watoto kadhaa, akiwemo Kutisa, Kinywaki na Kinanda. Kwa upande wa Mkomanile, alizaa mtoto mmoja pekee, binti aitwaye Maua, ambaye baadaye aliolewa na Jumbe Gomagoma. Hii ikawa mwanzo wa mkondo mpya wa historia.
Safari ya Uongozi
Baada ya kifo cha Pambuka, nafasi ya utawala ilichukuliwa kwa muda na Nchuranjunga, maarufu kwa mchezo wa jadi wa Nchuwa, unaofanana na Bao. Lakini hatimaye, Mkomanile alitawazwa rasmi kuwa chifu wa Undendeule.
Kuwa mtawala mwanamke katika jamii yenye mfumo wa kiukoo wa kiume lilikuwa jambo la kipekee mno. Lakini Mkomanile alionekana si tu kiongozi wa kaya, bali aligeuka kuwa nguzo ya ujasiri wa kijamii na kisiasa.
Wakati huo, Wajerumani walikuwa wakitawala Afrika ya Mashariki wakiwa na sera za ukatili:
Mikakati ya kikatili ya kikoloni ndiyo iliyosababisha kuibuka kwa vuguvugu la mapambano kama vile Vita ya Majimaji (1905–1907). Hapo ndipo jina la Mkomanile likajikita.
Mkomanile na Kinjeketile: Ndoa ya Kijeshi na Kiroho
Katika enzi ya utawala wake, alifika kijana mwenye haiba na ushawishi mkubwa kutoka Liwale, mkoani Lindi – Kinjeketile Ngwale.
Awali alijipenyeza kama mtumishi katika ikulu ya Mkomanile. Baadaye, kupitia elimu ya tiba na mazingaombwe, walizidi kuwa karibu hadi kuishi kama mume na mke.
Kinjeketile alimshawishi Mkomanile na watu wake kugoma kufanya kazi za kulazimishwa mashambani na kuamini kuwa risasi za Wajerumani zingekuwa maji endapo wangepigana kwa imani na mshikamano.
Ilikuwa ni falsafa iliyoamsha ari ya mapambano kusini mwa Tanzania.
Mapambano na Usaliti
Hatua ya kugoma kwa watu wa Undendeule iliwakera sana Wajerumani. Jeshi lao chini ya Kamanda Von Zelewski, liliwakamata watoto na watu wa kifalme wa Mkomanile, akiwemo binti yake Maua na mkwe wake Gomagoma.
Mkomanile, akijua kuwa watu wake walikuwa hatarini, alijisalimisha kwa hiari ili kuwaokoa. Msafara wake ulipofika Mlima Mkomanile, alifanya tambiko kwa ngoma ya Ihenja, ngoma maarufu ya kifalme, kama ishara ya ujasiri na ibada ya kiroho.
Lakini askari wa Kijerumani walipomkamata, walimnyonga mara mbili na kitanzi kikakatika mara zote. Tukio hili liliwaacha Wajerumani wakiwa na mshangao mkubwa. Hatimaye, kwa hasira, walimpiga risasi tatu tumboni na kumkata kichwa. Kichwa hicho walichukua hadi Ujerumani, na hadi leo hakijawahi kurejeshwa.
Hivyo ndivyo simulizi la Chifu Mkomanile lilivyofikia kilele chake cha kusikitisha, lakini pia cha kishujaa.
Urithi na Mafunzo
Hadithi ya Mkomanile ni ushahidi kwamba wanawake nao walikuwa mstari wa mbele katika mapambano ya ukombozi. Wakati historia nyingi zikimsimulia Kinjeketile, jina la Mkomanile limeachwa nyuma.
Kwa hakika, yeye ndiye mfano wa kwamba mapambano ya ukoloni hayakuwa ya wanaume pekee, bali ni ya jamii nzima.
Kwa mujibu wa wanahistoria wa Ruvuma, hadi leo kuna simulizi kwamba kiwiliwili cha Mkomanile hakikupatikana kamwe, jambo linaloongeza taswira ya kifumbo katika historia yake. Warithi wa ukoo wa Fussi walikuja kuendelea na uongozi hadi miaka ya uhuru, ambapo jina la mwisho lililojulikana ni Efrem Juta Luambano.
Hadithi ya Chifu Nduna Baina Mkomanile ni simulizi ya ujasiri, uzalendo na hekima. Ni hadithi ya mwanamke aliyepigana sio kwa upanga pekee, bali pia kwa imani, tambiko na mshikamano wa kijamii.
Ingawa kichwa chake bado kipo ugenini, roho yake imebaki kuwa nguzo ya kumbukumbu za ukombozi.
Ni wajibu wa taifa letu kuhakikisha majina kama yake hayapotei kwenye vumbi la historia. Kama ilivyo kwa mashujaa wengine, Mkomanile anastahili kurejeshwa heshima yake katika historia ya kitaifa na kikanda.

Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.