Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Crispin Chalamila, amewasili mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi ya siku kadhaa yenye lengo la kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa na kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma.
Kulingana na ratiba ya ziara yake Oktoba 9, Bw. Chalamila ataongoza uzinduzi wa jengo jipya la ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Nyasa, mradi unaolenga kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza ufanisi wa kiutendaji.
Akizungumza jana mjini Songea baada ya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, Chalamila alisema licha ya changamoto ya upungufu wa watumishi ikilinganishwa na ukubwa wa mkoa wa Ruvuma, taasisi yake imeendelea kufanya kazi kwa weledi kutokana na ushirikiano wa karibu kutoka kwa viongozi wa serikali na wadau wa maendeleo.
“Tumejipanga kuongeza nguvu kwenye kuzuia rushwa kabla haijatokea. Tunafanya hivyo kwa kutoa elimu kwa umma ili wananchi watambue madhara ya rushwa na wajue wajibu wao katika kulinda mali ya umma,” alisema Chalamila.
Aliongeza kuwa TAKUKURU ina jukumu la kuzuia, kuchunguza na kutoa elimu dhidi ya rushwa, na mkazo wa sasa ni kuzuia upotevu wa rasilimali kwa kupitia kampeni za elimu vijijini na mijini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, alisema ziara ya Chalamila ni ishara ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupambana na rushwa kwa vitendo.
“Ujenzi wa ofisi mpya za TAKUKURU katika wilaya ya Nyasa ni hatua muhimu ya kuimarisha uwajibikaji. Tunataka kila mwananchi awe karibu na taasisi hii ili kurahisisha utoaji wa taarifa na kufuatilia miradi yao ya maendeleo,” alisema Brigedia Jenerali Abbas.
Alibainisha kuwa mkoa wa Ruvuma umeweka mfumo wa vituo vya taarifa na vikao vya ushirikishwaji vinavyowawezesha wananchi kushiriki katika ufuatiliaji wa miradi.
Aidha, Chalamila alisisitiza kuwa ujenzi wa ofisi ya TAKUKURU Nyasa ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kuboresha miundombinu ya taasisi hiyo, ambapo ofisi 14 mpya zinatarajiwa kukamilika kote nchini ifikapo mwisho wa mwaka 2025.
“Tunataka kila wilaya nchini iwe na ofisi ya kudumu ya TAKUKURU ifikapo mwaka 2026. Hii itarahisisha mapambano ya rushwa katika ngazi zote,” alisisitiza.
Kwa sasa, mkoa wa Ruvuma una ofisi za TAKUKURU katika wilaya zote isipokuwa mbili, na ujenzi wa ofisi hizo unaendelea. Wananchi wa Nyasa wameelezwa kuwa uzinduzi wa ofisi yao mpya utarahisisha upatikanaji wa huduma na kuimarisha uchunguzi wa tuhuma za rushwa katika miradi ya maendeleo.

Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.