Katika kurasa za historia ya ukombozi wa Afrika, majina ya Mtemi Mkwawa na Kinjeketile Ngwale yameandikwa kwa wino mzito. Lakini je, umewahi kusikia jina la Chifu Nduna Baina Mkomanile – mwanamke jasiri kutoka Undendeule kijiji cha Kitanda wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, aliyeongoza mapambano dhidi ya ukoloni wa Kijerumani mwishoni mwa karne ya 19?
Mkomanile hakuwa tu chifu, bali alikuwa nembo ya ujasiri, hekima na uimara wa mwanamke wa Kiafrika. Akiwa mganga na mtawala, aliongoza jamii yake kupinga ukatili wa Wajerumani kwa ari isiyotetereka. Kwa ushirikiano na Kinjeketile Ngwale, aliwasha moto wa mapambano ya Maji Maji (1905–1907), akiwahamasisha watu kuamini kuwa uhuru unaweza kupatikana kupitia imani, umoja na tambiko za jadi.
Lakini ushupavu wake ulimgharimu maisha. Wajerumani walimnyonga mara mbili bila kufa—kisha wakampiga risasi na kumkata kichwa chake kilichopelekwa Ujerumani, ambako hadi leo hakijarudishwa.
Urithi wa Mkomanile unaendelea kuishi kupitia shule, makumbusho na simulizi za wazee wa Kitanda. Ni kielelezo cha mwanamke aliyeinua sauti ya kizazi chake – akithibitisha kwamba ukombozi wa Afrika haukuandikwa na wanaume pekee.
Ni wakati sasa Tanzania na dunia kumrejeshea heshima yake – kwani historia isiyomtaja Mkomanile ni historia isiyo kamili.

Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.