Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amesema wataalamu kutoka hospitali maalumu ya taifa ya magonjwa ambukizi ya Kibong’oto, wataendesha uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa wachimbaji wa madini na jamii zinazozunguka migodi kuanzia Oktoba 6 hadi 10.
Akifungua kikao kazi cha wataalamu kuhusu athari za vumbi la silica na magonjwa ya mapafu kwa jamii za wachimbaji wa madini, kilichofanyika katika ukumbi wa Songea Club, mjini Songea, amesema huduma hiyo itahusisha utoaji wa elimu ya afya kuhusu magonjwa ya mapafu yanayosababishwa na vumbi, hasa katika mazingira ya migodini.
“Zoezi hili pia litahusisha uhamasishaji wa jamii katika kudhibiti visababishi vya magonjwa sugu ya mapafu na kuimarisha mfumo wa uchunguzi wa mapema. Nitoe wito kwa wataalamu wote watakaopata fursa hiyo kuijitoa bila kuchoka ili kuhakikisha zoezi hili linafanyika kwa mafanikio makubwa,” alisema Brig. Jen. Ahmed.
Ameipongeza hospitali ya Kibong’oto kwa ushirikiano wao na serikali, akisema ni nyenzo muhimu katika kujenga mbinu madhubuti za kinga, uchunguzi na tiba kwa jamii hasa kwa magonjwa ambukizi kama kifua kikuu na yanayotokana na vumbi la migodini ikiwa Ruvuma ni moja ya mikoa yenye migodi ya madini.
Naye Mkurugenzi wa Hospitali ya Kibong’oto, Dkt. Leonard Subi, amesema uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu utafanyika kupitia huduma ya kliniki inayotembea (Mobile Clinic) katika halmashauri za Songea na Mbinga, pamoja na maeneo ya migodi ya makaa ya mawe yaliyopo mkoani Ruvuma.
Ameeleza kuwa huduma hiyo itatolewa bila malipo, na kwa wale watakaobainika kuwa na ugonjwa huo, watapatiwa matibabu na kuunganishwa na vituo vya afya pale inapohitajika.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mary Makondo, amesema uwepo wa wataalamu hao mkoani humo ni ushahidi wa dhamira ya pamoja ya wadau wa maendeleo katika kulinda afya za wananchi katika kuhakikisha shughuli za kiuchumi, ikiwemo uchimbaji wa madini, haziwi chanzo cha madhara kwa jamii.
Mpango huo unalenga kuhakikisha afya za wachimbaji wa madini na jamii zinazowazunguka zinalindwa ipasavyo kwa kuwa ndio walio kwenye hatari zaidi ya kuathirika na vumbi la migodini.

Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.