Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Crispin Francis Chalamila, amewasili mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi ikiwemo kuzindua jengo jipya la ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Nyasa.
Katika mazungumzo yake na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, yaliyofanyika ofisini kwake mjini Songea, Bw. Chalamila ameeleza kuwa licha ya changamoto ya upungufu wa watumishi ikilinganishwa na ukubwa wa mkoa, utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo umekuwa ukitegemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa ngazi mbalimbali na wadau wa maendeleo katika mkoa.
Bw. Chalamila amewahimiza viongozi wa mkoa kuendeleza mshikamano na kutoa usaidizi kwa TAKUKURU ili taasisi hiyo iendelee kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kwa kuzingatia weledi.
Amesema TAKUKURU ina jukumu la kuzuia rushwa, kutoa elimu kwa umma na kuchunguza ubadhilifu wa rasilimali, hivyo kwa sasa, taasisi hiyo imeweka mkazo kwenye kuzuia rushwa kwa kutoa elimu, hatua itakayosaidia kuepuka hasara kutokana na ubadhilifu wa mali za umma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, ameeleza kuwa ziara hiyo ni ishara ya dhamira ya serikali katika kuimarisha vita dhidi ya rushwa akisema uwekezaji katika miundombinu ya TAKUKURU, ikiwemo ujenzi wa ofisi za wilaya, ni hatua muhimu katika kusogeza huduma karibu na wananchi, kuimarisha uwajibikaji, na kuongeza ufanisi wa usimamizi wa miradi ya maendeleo.
Pamoja na mambo mengine amemuhakikishia Mkurugenzi wa TAKUKURU kuwa mkoa wa Ruvuma unatambua mchango mkubwa wa taasisi hiyo katika kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali za umma na kuendeleza utawala bora.
Amebainisha kuwa mkoa huo umejenga utamaduni wa kushirikiana kwa karibu na TAKUKURU, ikiwemo kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa uwazi na wananchi wanashiriki kikamilifu katika ufuatiliaji kupitia vituo vya taarifa na vikao vya ushirikishwaji.

Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.