Benki ya NMB imeendelea kuonesha mfano wa taasisi ya kifedha inayogusa maisha ya Watanzania baada ya kuadhimisha kwa mafanikio makubwa “Siku ya Kijiji” (Village Day) katika Kata ya Mbesa, Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma tukio lililojaza hamasa, burudani na matumaini mapya kwa wananchi.
Shughuli hiyo iliyofanyika Oktoba 4 mwaka huu, ilianza alfajiri kwa mazoezi ya kukimbia (jogging) yaliyowashirikisha mamia ya wakazi wa Mbesa, watumishi wa serikali, wafanyakazi wa NMB na wanafunzi. Baadaye, umati wa watu ulijumuika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mbesa kwa mazoezi ya viungo, michezo na burudani mbalimbali zilizofufua ari ya ushirikiano na afya bora kwa jamii.
Mamia ya watu walihudhuria maadhimisho hayo yaliyopambwa na michezo ya kuvuta kamba, kukimbiza kuku, mpira wa miguu na michezo ya watoto. Lengo kuu, kwa mujibu wa NMB, ni kujenga uhusiano wa karibu na wateja pamoja na kuhamasisha matumizi ya huduma za kifedha kwa jamii za vijijini.
Akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mheshimiwa Denis Masanja, alitoa pongezi kwa Benki ya NMB kwa ubunifu wake wa kuwaleta pamoja wananchi kupitia shughuli za kijamii.
“Benki ya NMB inatoa mfano bora wa taasisi inayowekeza si tu katika huduma za kifedha, bali pia katika ustawi wa jamii. Hii ni benki inayogusa maisha ya watu kwa vitendo,” alisema Mhe. Masanja huku akishangiliwa na wananchi.
DC Masanja aliipongeza NMB kwa hatua yake ya kukipatia Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) cha Chichilimbe mkopo wa kununua gari la mizigo, akibainisha kuwa hatua hiyo itarahisisha usafirishaji wa mazao ya wakulima hadi maghala makuu kwa wakati, jambo litakaloongeza kipato cha wanachama.
Kwa upande wake, Meneja wa NMB Kanda ya Kusini, Bi. Olipa Hebel, alieleza kufurahishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi wa Mbesa, akisema tukio hilo linaonesha jinsi jamii inavyotambua umuhimu wa ushirikiano na taasisi za kifedha.
“Tunapofika kijijini, tunaleta zaidi ya huduma za kibenki tunaleta elimu, afya, na furaha. NMB ipo kwa ajili ya wananchi wote, kuanzia mjini hadi vijijini,” alisema Bi. Hebel.
Katika maadhimisho hayo, NMB ilitoa elimu ya fedha kwa vikundi vya wajasiriamali, wakulima na vijana, ikiwahimiza kutumia huduma za kibenki kwa usalama wa fedha na upatikanaji wa mikopo midogo ya maendeleo.
Yasini Msyano, Meneja wa Chama cha Ushirika cha Chichilimbe, aliishukuru NMB kwa kuonesha imani kubwa kwa chama hicho.
“Kupata gari hili ni hatua kubwa. Tutatumia vizuri mkopo huu ili kuhakikisha mazao ya wakulima yanafika sokoni kwa wakati. Hii ni neema kwa kijiji chetu,” alisema Msyano.
Kwa mujibu wa takwimu za NMB, zaidi ya vikundi 200 vya wakulima katika Mkoa wa Ruvuma vimenufaika na mikopo na elimu ya fedha kupitia mpango wa NMB Vijijini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita .

Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.