Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mary Gasper Makondo, ameziagiza halmashauri ambazo bado hazijakamilisha zoezi la umezeshaji dawa kingatiba za usubi kuhakikisha zinatekeleza jukumu hilo kabla ya mwezi Desemba 2025.
Ametoa maagizo hayo wakati akifungua kikao kazi cha mpango mkakati wa umezeshaji dawa kingatiba kwa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, kilichofanyika katika ukumbi wa Songea Club, mjini Songea.
“Ninazipongeza baadhi ya halmashauri kwa kufanikisha zoezi la umezeshaji dawa kingatiba za usubi baada ya kupokea maagizo kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa kulingana na ratiba ya zoezi, kwa halmashauri ambazo bado hazijamezesha dawa kingatiba za usubi zinapaswa kufanya hivyo kabla ya mwezi Desemba 2025,” alisema Makondo.
Makondo amewataka wataalamu kuhakikisha kikao hicho kinajadili na kuandaa mpango mkakati utakaowezesha umezeshaji wa dawa kingatiba katika ngazi ya jamii na shule, akisisitiza mkoa unatarajia kuendesha zoezi la umezeshaji dawa kingatiba za kichocho na minyoo tumbo kwa watoto wenye umri wa kwenda shule kuanzia Januari 2026.
Pamoja na hayo, amewataka wakurugenzi wa halmashauri kwa kushirikiana na wataalamu wao kuona namna ya kupata fedha zitakazowezesha kufanikisha zoezi hilo katika ngazi ya shule na jamii, akisisitiza kuwa utekelezaji wake unatakiwa kufanyika kwa kutumia rasilimali zilizopo ndani ya halmashauri.
Akihitimisha kikao hicho kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Louis Chomboko, amesisitiza kuwa taifa haliwezi kujenga uchumi imara bila kuwa na jamii yenye afya bora.
Amebainisha kuwa kuzuia na kudhibiti magonjwa ni msingi wa kulinda nguvu kazi ya taifa, kupunguza gharama za matibabu kwa familia na serikali, na hivyo kuchochea maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.