Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya urejeshaji wa mawasiliano katika daraja la Mto Mnywa Maji, lililopo kijiji cha Ruanda wilayani Mbinga, baada ya kusombwa na maji kufuatia mvua kubwa.
Akiwa katika ziara hiyo, RC Ahmed ameeleza kuwa daraja hilo ni kiungo muhimu kwa shughuli za kiuchumi, ikiwemo usafirishaji wa makaa ya mawe na shughuli nyingine za wananchi. Amesisitiza kuwa ndiyo maana serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni tatu katika ujenzi wa daraja hilo pamoja na barabara ya Kitai–Ruanda.
Ameeleza kuwa changamoto zinazojitokeza katika daraja hilo ni majanga ya asili na si uzembe wa mtu yeyote. Akisisitiza kuwa serikali ipo bega kwa bega na wananchi kuhakikisha shughuli za kiuchumi na kijamii zinaendelea bila kukwama.
Pamoja na mambo mengine ametoa pongezi kwa Wakala wa Barabara Mkoa wa Ruvuma (TANROADS) pamoja na mkandarasi kwa kazi kubwa ya kurejesha mawasiliano katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Salehe Juma, ametoa tahadhari kwa wasafirishaji wa makaa ya mawe kutozidisha uzito wa mizigo.
Ameeleza kuwa madaraja ya muda yaliyopo kwa sasa hayawezi kuhimili mizigo mizito, hivyo wasafirishaji wanashauriwa kubeba tani 25 hadi 30 pekee ili kulinda miundombinu ya muda wakati serikali ikiendelea na ujenzi wa daraja la kudumu katika eneo hilo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.