Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema kuwa ili Mkoa wa Ruvuma upate matokeo zaidi katika sekta ya kilimo, ni lazima maonesho ya Nane Nane ya Mkoa yaboreshwe ili kuleta tija kwa wananchi.
Akifunga maonesho hayo kimkoa ambayo yamefanyika katika viwanja vya Amani Makolo, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Kanali Ahmed amesema kuwa Mkoa wa Ruvuma umeongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kwa miaka sita mfululizo, hivyo kuna kila sababu ya kuboresha maonesho hayo ili yawe chachu ya maendeleo kwa wakulima.
"Tuna uhakika wa kupiga hatua mpya zaidi katika kuboresha na kukuza uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu, madini, nyuki, ushirikiano na kuhamasisha utalii katika mkoa wetu, sina mashaka kuwa elimu iliyopatikana mwaka huu itaufanya Mkoa wa Ruvuma kuendelea kuwa miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri katika uzalishaji wa mazao mbalimbali nchini hususan mazao ya chakula," amesema Kanali Ahmed.
Amewaagiza waandaaji na waratibu wa maadhimisho hayo kuhakikisha wanawashirikisha wadau mbalimbali ili kuongeza teknolojia za kisasa za kilimo zinazohitajika katika maonesho hayo ikiwa lengo ni kutoa elimu stahiki kwa wananchi ili wanufaike na maarifa hayo katika kuongeza tija kwenye shughuli zao za kilimo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mhe. Kisare Makori, amesema kuwa katika kuhakikisha wanaboresha shughuli za kilimo, tayari wataalam wapo wilayani humo wakifanya usanifu wa awali kwa ajili ya kuanzisha mabwawa makubwa ya umwagiliaji akieleza kuwa mabwawa hayo yatatoa fursa kwa wananchi kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo, biashara na chakula.
Mratibu wa Maadhimisho ya Nane Nane Mkoa wa Ruvuma, Ndugu Onesmo Paul, ameeleza kuwa zaidi ya tani milioni mbili za mazao nchini zimezalishwa kutoka Mkoa wa Ruvuma kwa msimu wa kilimo uliopita wa mwaka 2024/25, wakati matumizi ya mbolea yalikuwa zaidi ya tani laki moja, huku zaidi ya asilimia 20 ya wakulima wa Mkoa wa Ruvuma wanatumia mbegu bora, hususan kwa zao la mahindi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.