Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mheshimiwa Kapenjama Ndile, amebainisha kuwa hadi kufikia mwezi Julai, 2024 Mkoa wa Ruvuma umezalisha tani 2,052,449 za mazao ya chakula.
Amesema hayo wakati akifungua kongamano la kilimo biashara lililofanyika katika ukumbi wa kanisa Katoliki Parokia ya Bombambili mjini Songea akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed.
"Nchi imezalisha tani Milioni 8, Mkoa wa Ruvuma tumezalisha tani Milioni 2 unaweza kuona sisi sio wadogo tuna mchango mkubwa katika sekta ya kilimo" alisema Kapenjama Ndile.
Katika kongamano hilo Maafisa Ugani wamepatiwa Vishikwambi kwa ajili ya kuwawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na kuongeza tija katika kilimo, ambapo amewataka Maafisa hao kuvitumia vifaa hivyo vinavyotolewa na Wizara ya Kilimo vikiwemo Vishikwambi na pikipiki kwa matumizi sahihi na yaliyokusudiwa.
Naye Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Ndg. Jumanne mwankhoo ameliyataja lengo la kongamano ni kujiweka sawa kuelekea msimu wa kilimo 2024/25 ndio sababu ya wadau mbalimbali wa kilimo yakiwemo Makampuni ya wauzaji wa pembejeo na mbolea kujumuika.
Ameeleza kuwa kilimo biashara ni kilimo kinachotoa faida, hivyo amewasisitiza wakulima kuweka mipango ya kilimo mapema na kuacha kulima kwa mazoea.
Kwa upande wake Afisa Kilimo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Onesmo Ngao, ameishukuru Selous FM kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuandaa kongamano la kilimo biashara na kulitaja kama kielelezo na chachu kwa wakulima hususani kuelekea katika msimu mpya wa kilimo.
Kongamano la kilimo biashara kimefanyika mara ya pili mwaka huu ambapo mara ya kwanza lilifanyika mwaka 2023 ikiwa ni sehemu ya juhudi za wadau wa kilimo kuboresha mbinu za uzalishaji na kuongeza tija katika sekta ya kilimo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.