Mkuu wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Mhe. Kapenjama Ndile, amempongeza kwa dhati Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Wakili Muhoja, kwa uamuzi wa kizalendo wa kutoa bajeti ya shilingi milioni 61 kugharamia ushiriki wa watumishi wa halmashauri hiyo katika mashindano ya SHIMISEMITA kitaifa 2025, yaliyoanza tarehe 15 Agosti 2025, jijini Tanga.
Akizungumza katika kikao maalum kilichofanyika kwenye viunga vya Halmashauri ya Manispaa ya Songea, DC Ndile alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa sera ya michezo ya taifa pamoja na agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linalozitaka wizara, taasisi na idara za serikali kuunda mashirikisho ya michezo kwa watumishi wa umma.
“Mji wa Songea una historia kubwa ya michezo, hususan kupitia timu ya Majimaji na Uwanja wa Majimaji. Historia hii iliasisiwa na hayati Dkt. Lawrence Gama, aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na mpenda michezo hodari. Tunayo dhamana ya kuendeleza urithi huu wa kifahari,” — alisema Mhe. Ndile.
DC Ndile aliwataka wanamichezo kuonesha nidhamu, ustaarabu, bidii na umoja wakiwa uwanjani, huku akiahidi zawadi nono iwapo timu hiyo itarejea Songea ikiwa na ngao ya ushindi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Wakili Muhoja alisema bajeti ya milioni 61 iliyotengwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 itagharamia usafiri, posho, vifaa vya michezo na ada za ushiriki. Pia aliahidi kuongeza idadi ya michezo kwa bajeti ya 2026/2027, ikiwemo kwaya na michezo mingine ya burudani.
Miongoni mwa michezo itakayoshirikisha watumishi wa Manispaa ya Songea ni:
Mpira wa miguu
Mpira wa pete
Mpira wa wavu
Kuvuta kamba
Drafti
Bao la Kiswahili
Nahodha wa timu, akizungumza kwa niaba ya wanamichezo wote, aliwashukuru viongozi wa Halmashauri na Wilaya kwa jitihada za kuwawezesha kushiriki mashindano hayo, huku akiapa kuwa Songea itarudi na ushindi wa kishindo!
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.