Kuelekea maadhimisho ya miaka 26 tangu kufariki kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Songea imefanya zoezi la usafi ikiwa ni sehemu ya kumuenzi kiongozi huyo.
Zoezi hilo limefanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Songea (Homso) pamoja na Soko Kuu la Songea, likihusisha ushiriki wa klabu ya madaktari, wanamichezo, wasanii wa ngoma za asili, na wadau mbalimbali kutoka maeneo tofauti.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa zoezi la usafi, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Jumanne Mwankhoo, amesema kuwa maadhimisho hayo ni fursa kwa wananchi kujitathmini na kuenzi misingi ya kazi na demokrasia aliyoasisi Mwalimu Nyerere.
Pamoja na mambo mengine amewahimiza wananchi kujituma katika shughuli za maendeleo na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Louis Chamboko, amesema kuwa usafi wa mazingira ni nguzo muhimu ya afya ya jamii akisisitiza kwa kudumisha usafi, wananchi wataweza kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Amesema kutakuwa na huduma za bure za upimaji wa afya kwa wananchi, ambapo watachunguzwa magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu, kiwango cha sukari mwilini, uzito pamoja na hali ya lishe ambapo zoezi hilo linafanyika katika viwanja vya Soko Kuu la Songea, na litahitimishwa tarehe 14 Oktoba katika viwanja vya Majimaji.

Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.