Katika shamrashamra za Wiki ya Huduma kwa Wateja 2025, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Ruvuma limeweka historia mpya kwa kufanya ziara maalum wilayani Mbinga, likiwatunuku wateja wake wanaotumia nishati safi ya umeme katika shughuli za uzalishaji.
Kupitia tukio hilo, TANESCO imekabidhi masufuria ya kisasa ya kupikia kwa umeme (pressure cookers) kwa mama lishe, tokeni za LUKU kwa wajasiriamali wa saluni, na zawadi ya umeme wa bure kwa shule ya sekondari ya Mbinga, ili kusaidia wanafunzi wa bweni kujiandaa na mitihani yao.
Afisa Uhusiano wa TANESCO Ruvuma, Alan Njiro, amesema hatua hiyo inalenga kuhamasisha matumizi ya nishati salama, nafuu na rafiki kwa mazingira, akibainisha kuwa masufuria hayo yanapunguza gharama za uendeshaji na kulinda afya za watumiaji.
Kwa upande wake, Mhandisi Edward Kweka, Meneja wa TANESCO Mbinga, amehimiza wananchi kutumia vifaa hivyo kwa ufanisi na kutoa taarifa mara moja kwa namba 180 endapo kutatokea hitilafu za umeme.
Mama lishe Regina Komba na Mama Sania waliopokea zawadi hizo, wametoa shukrani kwa TANESCO kwa kuwawezesha kupunguza gharama za mkaa kutoka Tsh 1,000 hadi chini ya Tsh 250 kwa mlo mmoja.
TANESCO Ruvuma imeonesha dhamira thabiti ya kuwasha maendeleo kupitia nishati safi, chini ya kaulimbiu “Mpango Umewezekana”.

Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.