Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Mhe. Ngolo Malenya, amesema Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum imeanza kushughulikia changamoto za wajasiriamali wadogo ikiwemo upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu inayotolewa na Serikali kupitia Benki ya NMB.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, wakati akifungua kongamano la wafanyabiashara ndogo ndogo Mkoa wa Ruvuma lilillofanyika katika ukumbi wa Songea Club mjini Songea, Mhe. Ngolo Malenya amebainisha kuwa hata mtu mmoja mmoja anaweza kukopa bila ya kuwa na kikundi.
"Hii ni fursa pekee kwa mtu binafsi kukopa mwenyewe na kuhakikisha anarudisha mkopo huo, maana tunajua kwenye mikopo ya vikundi huwa ina changamoto, unakuta Serikali inadai wakati watu wameshindwa kulipa, na wengine wakipata hiyo mikopo wanatumia kwa ajili ya shughuli zao," alisema Mhe. Malenya.
Amesema kuwa ili mfanyabiashara aweze kupata mikopo hiyo ni lazima awe amepata kitambulisho cha mjasiriamali mdogo ambapo usajili huo unafanyika katika halmashauri zote za mkoa wa Ruvuma kupitia maafisa wa maendeleo ya jamii na maafisa wa biashara.
Katika hatua nyingine ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kuhakikisha wanatoa hamasa kwa wafanyabiashara ili waweze kuchukua mikopo hiyo kwa kuwa rekodi za mkoa zinaonesha kuwa Halmashauri hiyo haijatoa mikopo hiyo.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mariam Juma, akitoa taarifa ya wafanyabiashara ndogondogo mkoa, amesema hadi kufikia Julai 2025 wafanyabiashara waliosajiliwa ni 2,222 huku waliopokea vitambulisho vya wajasiriamali wadogo ni 975 pekee, hivyo ametoa wito kwa wafanyabiashara kuhakikisha wanajisajili na kupata vitambulisho kwa kuwa ndivyo vitakavyowawezesha kupata mikopo hiyo ya riba nafuu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.