Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Manunuzi kutoka halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma wamepatiwa mafunzo ya usajili na uwezeshaji wa makundi maalum kapitia fursa za ununuzi wa umma.
Afisa Ununuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Bw. Amiri Mhando, amesema lengo la serikali ni kuhakikisha maafisa maendeleo ya jamii wanashiriki kikamilifu katika kuibua na kusajili makundi maalum akibainisha kuwa maafisa maendeleo ya jamii na maafisa vijana ndio wanaohusiana moja kwa moja na kundi kubwa la watu katika jamii.
Amesema hatua hiyo ni msukumo wa serikali katika kutengeneza fursa za kijamii ili kuondoa umaskini. Ameongeza kuwa juhudi hizo zimekuwa zikisaidia watu wengi kujiajiri na kujiongezea kipato kupitia njia halali za ununuzi wa umma.
Kwa upande wake, Afisa TEHAMA Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Bw. Damas Makweba, amewataka maafisa hao kutoa elimu kwa makundi maalum. Pia amewahimiza wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa zinazotolewa na serikali.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mariam Juma, amesema mafunzo hayo yatasaidia kujenga uwezo wa kuunda makundi mengi na kushiriki kwenye fursa za ununuzi wa umma.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuongeza idadi ya makundi maalum yatakayosajiliwa kwenye mfumo na kuwaonyesha wananchi namna ya kujiongezea kipato na kuboresha maisha ya familia na taifa kwa ujumla.
Kwa upande mwingine, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Bi. Cecilia Mbata, amesema mafunzo hayo yatawasaidia kuyafikia makundi mengi zaidi ili yaweze kupata na kunufaika na fursa za serikali.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.